Powered By Blogger

Sunday, August 7, 2011

Ajinyonga kwa kuchoshwa na vipigo vya Mkewe.

MKAZI mmoja katika Mtaa wa NHC katika Mji wa Mugumu wilaya ya Serengeti wilayani Mara, Samson Kitoshi (32) amejinyonga hadi kufariki dunia kwa kamba chumbani kwake kwa kile alichodai kuwa: “Amechoka kupigwa na mkewe kila wakati.”

Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa watu, linadaiwa kutokea jana saa tano asubuhi. Akisimulia mkasa huo, mtoto wa marehemu (Jina tunalihifadhi) alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo, mama yao alimpa Sh 1,000 akanunue sukari na vitafunio, lakini asimpe baba yao chai... "Mama aliaga kuwa anakwenda Hospitali DDH kwa kuwa anaumwa. Baba akasema hatakunywa chai hiyo na kutuambia kuwa hatutamwona tena anatuaga na tusiingie ndani."

Marehemu baada ya kuingia chumbani kwake anadaiwa kuwa alifunga kamba juu ya dari na kujining'iniza hadi alipokata roho.Mtoto huyo wa darasa la tatu ambaye ana umri wa miaka 10 alisema hawakuweza kuingia ndani kama walivyoambiwa na baba yao, lakini baadaye aliamua  kumwamsha akidhani kuwa amelala ili anywe chai ndipo alipokuta amening'inia. Alipiga kelele kuomba msaada.

"Baba alikuwa amevua shati akawa amening'inia chini kuna meza nikaweka stuli ili nifungue kamba sikuweza nikapiga yowe majirani wakafika wakasema ameshakufa," alisema.

Kuhusu migogoro ya ndani, mtoto huyo alisema kumekuwa na ugomvi wa mara kwa mara hasa ukisababishwa na mama yao ambaye anauza pombe ya kienyeji ya wanzuki anaporudi akiwa amelewa kwani humfanyia vurugu baba yao.

"Hivi karibuni baba alifikia hatua ya kumtaka mama aondoke amechoka na mateso anayomfanyia, lakini mama alikataa kuwa hawezi kutoka na kudai yeye ndiye atakayetoka," alisema.Ndugu wa Kitoshi ambaye anaishi katika Kijiji cha Morotonga alisema kuwa marehemu aliyekuwa akifanya kazi ya kusaga nafaka alikuwa akilalamika kupigwa na mkewe mara kwa mara.

"Huyu ni ndugu yangu hata leo amefika kwangu na akanikosa na kurudi nadhani alitaka kuniambia kitu. Baada ya muda nikapigiwa simu kuwa amekufa kwa kujinyonga, amechoshwa na kupigwa," alisema.

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Serengeti, Paulo Mng'ong'o alijaribu kumtafuta mwanamke huyo kwa simu lakini mara baada ya kujitambulisha kuwa yeye ni OCD, mama huyo alikata simu.

Baada ya muda mama huyo alifika nyumbani na kumkuta mume wake akining'inia kwenye kamba. Huko alipokewa kwa maneno makali kutoka kwa wanawake wenzake waliokuwa na hasira baadhi wakisema: “Ulitaka afe ujitawale sasa amekufa tanua... unadanganya ulikuwa hospitali mbona umelewa..."

Maneno hayo makali yalimwingia mwanamke huyo kwani alikaa chini kisha akalala chali na kupoteza fahamu. Hakuweza kunyanyuka hadi alipopakiwa kwenye gari la polisi pamoja na mwili wa mumewe na kupelekwa hospitali.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Mng'ong'o alisema polisi inalifanyia uchunguzi na kwamba itatoa taarifa kwa umma. Alisema wangefanya mahojiano na mke huyo wa marehemu baada ya kuzinduka kujua chanzo cha kifo hicho.Mwenyekiti wa Mtaa wa NHC, Elias Nyamraba alisema kuwa wanasubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya hatua nyingine ikiwemo ya mipango ya mazishi akisema Kitoshi ni mzaliwa wa Kijiji cha Issenye.

No comments: