Powered By Blogger

Wednesday, July 6, 2011

Diwani, wengine 5 wauawa.

Imeripotiwa katika gazeti la Habari leo, kwamba watu sita akiwamo Diwani wa Lagangabilili wilayani Bariadi mkoani Shinyanga, kupitia chama cha United Democratic (UDP), wameuawa kikatili katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea saa 2.30 usiku katika kijiji cha Ng’esha wilayani hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema ofisini kwake jana kuwa, watu sita wakiwa na pikipiki tatu na bunduki moja ya kienyeji inayotumia risasi za shotgun waliwashambulia diwani Simba Sita (45) na Nyebu Kadundu (60) ambaye alikufa papo hapo.

Sita baada ya kupigwa risasi alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza, lakini akiwa njiani alipoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi. Inadaiwa majambazi hao walifyatua risasi ovyo kutawanya wananchi waliokuwa wakipiga kelele za kuomba msaada.

Katika tukio hilo, baada ya majambazi hao kufyatua risasi kadhaa walipora Sh milioni moja za Mduhu Sita (35) alizopata baada ya kuuza ng’ombe mnadani siku hiyo, Sh 55,000 na simu ya mkononi aina ya Nokia.

Kwenye duka la Mongo Maduhu kijijini hapo, walipora bidhaa za dukani zikiwamo betri za tochi na bidhaa nyingine ambazo idadi na thamani yao halisi bado haijafahamika na kuondoka kwa pikipiki tatu walizokuwa nazo na moja waliyopora kwa Diwani Sita aina ya Lifan namba T 693 BCN.

Kwa mauaji hayo ya kikatili, wananchi walikusanyika na kupiga kelele za kuomba msaada huku wakiwafuatilia majambazi hao kwenye vijiji jirani vya Lagangabilili, Gambasingu, Ipilililo, Kisesa na Giriku.

Baada ya msako na ufuatiliaji wa haraka, wananchi kwa kushirikiana na Sungusungu waliwaona wakiwa na pikipiki nne katika kijiji cha Kisesa, Meatu umbali wa kilometa saba kutoka eneo la tukio na wananchi kuwashambulia kwa mawe na marungu.

Kamanda Kamugisha alisema katika purukushani hiyo majambazi waliwaponyoka wananchi na kutelekeza pikipiki nne; namba T 664 BEQ, T 530 BDQ, T833 BFV zote aina ya Sunlag na namba T 693 BCN ya marehemu Diwani.

“Wananchi waliendelea kuwafuatilia majambazi hao huku wakiwashambulia kwa silaha za jadi na kusababisha vifo vya wanne na kufanya idadi ya waliouawa katika tukio hilo, kuwa sita hadi leo (jana),’’ alisema Kamugisha.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Nzungu Cherehani (50) mkulima wa kijiji cha Bukundi, Meatu; Sospeter James (40) wa mtaa wa Sima, Bariadi; Manjale Ngimba (40) mkulima wa kijiji cha Inalo, Bariadi na Jeremia Ntembe (35), mkazi wa kijiji cha Budalabujiga na Ng’esha, Bariadi, aliyeuawa jana na mwili wake kuteketezwa kwa moto. Kamugisha alisema, polisi wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.

No comments: