Baadhi ya watuhumiwa wakiwasili Mahakamani Kinondoni |
Wakisoma jana mashitaka mbele ya Hakimu Yohana Yongolo wa Mahakama hiyo, waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Leonard Swai na Pendo Temu, walidai kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Juni na Oktoba 2008.
Waliopandishwa kizimbani ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilongawima, Josephat Woiso, Diwani wa Kunduchi, Patrick Makoyola, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kilongawima Mbezi, Wanura Maranda na Mpima Ardhi Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Hamidu Mgaya.
Wengine ni Ofisa Mipango Miji wa Wizara hiyo, Anna Macha, Ofisa Mipango Miji Msaidizi wa Wizara, Mapambano Baseka na Ofisa Ardhi Msaidizi wa Manispaa ya Kinondoni, Saidi Maligwah. Mshitakiwa mwingine, Patrick Makoyola hakuwa mahakamani hapo.
Waendesha mashitaka hao walidai kuwa washitakiwa walitoa taarifa za uongo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, kuhusu viwanja na kusababisha aviidhinishe na kutoa hati halali.
Washitakiwa hao pia wanadaiwa kukiuka Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kwa kutumia madaraka yao vibaya na kusababisha watu kupata viwanja kinyume na utaratibu. Wote walikana mashitaka na wapo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana iliyowataka kuwa na wadhamini wawili wa kusaini dhamana ya Sh milioni moja kwa pamoja. Pia walitakiwa kutosafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali Julai 26 na Hakimu alitaka mtuhumiwa mwingine aliyesalia kufikishwa mahakamani pamoja na wenzake siku hiyo.
No comments:
Post a Comment