Powered By Blogger

Wednesday, June 22, 2011

DIWANI CCM JELA KWA KUTOA RUSHWA

DIWANI wa Viti Maalumu wa Tarafa ya mlingoti Wilayani Tunduru kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Atingala Mohamed amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya sh milioni 6 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa rushwa.

Katika shauri hilo namba 13/2011, Diwani huyo alituhumiwa kutoa khanga na vitenge kwa wajumbe 15 wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Tunduru ambapo alifanikiwa kuibuka mshindi wa nafasi hiyo. Mashtaka hayo yalifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, diwani huyo alikiuka kifungu Namba 13 (1) (A) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Bw. Sprian Semwija alisema kuwa mahakama hiyo imetoa adhabu hiyo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na inaamini kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia hiyo.Katika mashtaka hayo, Bi. Atingala alitiwa hatiani katika Makosa 9 kati ya 15 aliyokuwa akituhumiwa kuyafanya. Katika kosa la kwanza, mahakama hiyo ilimhukumu kutumikia kifungo cha miaka miwili Jela au kulipa faini ya sh. milioni mbili na makosa manane yaliyobakia mahakama hiyo ikamhukumu adhabu ya mwaka mmoja mmoja au kulipa faini ya sh. 500,000/ kwa kila kosa.

Wakizungumzia adhabu hiyo Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Bi. Monica Mtili mbali na kuonesha kushtushwa na taarfa za tukio hilo awliwataka viongozi Taasisi ya Kuzuwia na kupambana na Rushwa (PCCB) Mkoani Ruvuma kushughulikia na kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wa makosa ya Uchaguzi Mkuu wanafikishwa Mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake vingivyo wananchi watakosa imani na chombo hicho.

Nao Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Bw. Mustafa Bora na kaimu katibu wa CCM Wilaya ya Tunduru Bw. Hasan Kindamba walisema kuwa adhabu hiyo ni salamu kwa wanasiasa ambao hutumia njia za panya kupata madaraka na kuongeza kuwa ingawa makosa ya Rushwa yako wazi sana lakini kesi ya Diwani Atingala ilikuwa na mambo mengi yaliyojificha ingawa hawakufafanua.

Wakizungumzia nafasi ya udiwani viongozi hao walisema kuwa wanasubiri maelekezo kutoka Makao Makuu ya CCM taifa ili waweze kuteua Diwani mwingine kujaza nafasi hiyo.

Kamanda wa Taasisis ya Kuzuia na kupambana na Rushwa wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Daud Masiko alisema kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba watuhumiwa wote wa makosa ya uchaguzi watafikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.Chanzo gazeti la majira.

No comments: