Mhe. Mkuu wa Mkoa,
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama
Kuu,
Mheshimiwa Jaji Mstaafu, Jaji
Nchalla,
Mhe. Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu, Mwanza,
Mhe. Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu, Kitengo cha Biashara,
Mhe. Wakili wa Serikali Mfawidhi, Mwanza,
Mhe. Mwenyekiti wa Chama cha
Mawakili wa Kujitegemea Tawi la Mwanza,
Wah. Wastahiki Meya –
Nyamagana/Ilemela,
Wah. Wakuu wa Wilaya –
Nyamagana/Ilemela,
Wah. Mahakimu wa ngazi zote na
Wasaidizi wote wa Sheria wa Majaji,
Wah. Mawakili wote wa Serikali
na Kujitegemea,
Wah. Makamanda wa vyombo vya
Ulinzi, Magereza na Usalama wa Mkoa,
Wah. Viongozi wa Dini na Wakuu wa Taasisi
mbalimbali za Serikali mliopo,
Wah. Viongozi wote wa Vyama vya
Siasa,
Watumishi wote wa Mahakama wa
ngazi zote,
Wageni waalikwa, Mabibi na
Mabwana,
Itifaki imezingatiwa.
Wageni waalikwa mabibi na mabwana, awali ya yote napenda kuwatakia wote heri ya
mwaka mpya wa 2013. Aidha nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa kujumuika nasi katika sherehe hizi
za Siku ya Sheria ambayo ndio kiashiria cha kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama
mwaka huu. Najua mmeacha shughuli zenu za kawaida ili kujumuika nasi kufanikisha
sherehe hii. Nasema asanteni sana na karibuni sana.
Wageni waalikwa mabibi na mabwana Maudhui ya Siku ya Sheria ya mwaka huu ni “Utawala
wa sheria; Umuhimu na uimarishaji wake nchini”.
1.0
DHANA YA UTAWALA WA SHERIA
Hakuna tafsiri ya moja kwa moja ya maana ya
utawala wa sheria, kwani kihistoria
dhana ya utawala wa sheria ilianza zamani sana, na imepata tafsiri
tofauti kulingana na maendeleo katika Jamii. Wanazuoni na wanafalsafa maarufu
duniani, kama Aristotle, Dicey na John Locke na wengineo wengi wamejaribu kutoa tafsiri tofauti
tofauti juu ya utawala wa sheria, lakini tafsiri isiyo rasmi ya dhana nzima ya utawala
wa sheria yaani “Rule of law “- ni ule utawala
wenye kuheshimu usawa, uhuru wa watu, haki za binadamu pamoja na usawa mbele ya
sheria.
1.1
MISINGI YA UTAWALA WA SHERIA
Wageni
waalikwa mabibi na mabwana,
Ipo misingi mbalimbali ya utawala wa sheria,
ambayo jamii yoyote iliyostaarabika duniani sharti iifuate, misingi hii ndio
chimbuko la maendeleo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika jamii. Misingi hii ni kama ifuatayo:-
(i)
Usawa mbele ya Sheria yaani “Equality before the
Law”, Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,
1977 inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi
wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
(ii) Haki za
binadamu, jamii itahesabika kufuata
utawala wa sheria pale ambapo itazingatia na kuheshimu haki za binadamu. Haki
hizi ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya kuabudu, haki ya kusikilizwa, haki ya
faragha na usalama wa mtu na nyinginezo nyingi kama zilivyoainishwa katika
sehemu ya Tatu ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
(iii)Uhuru wa Mahakama- dhana ya utawala
wa sheria haiwezi kuwa timilifu kama Mahakama zetu nchini hazitakuwa
huru. Dhana ya uhuru wa Mahakama imebainishwa
wazi katika Ibara ya 107B ya Katiba
yetu ya 1977 tuliyonayo hivi sasa. Ibara hii inasema kuwa katika
“kutekeleza
mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia
tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi”.
Ibara hii ndio
chimbuko la uhuru wa mahakama Tanzania.
Ni vema nikagusia walau kwa muhtasari, sana
kuhusu dhana hii ya uhuru wa Mahakama.
Moja, mahakama ni mhimili wa dola
kati ya mihimili mitatu iliyopo. Mhimili huu unatakiwa uwe huru na mihimili
mingine yaani Serikali na Bunge haipaswi kuingilia uhuru huu kwa hali yoyote.
Na siyo mihimili hii tu hata asasi za kitaifa wala mtu yeyote hapaswi kuingilia
uhuru huu. Uhuru huu wa mahakama, kama papa avumavyo baharini, ndio unaovuma sana na pengine unakera
pia. Imejitokeza mara nyingi watendaji wa serikali kuingilia maofisa wa
mahakama katika kutekeleza majukumu yao
ya kila siku. Ipo mifano mingi sana, mfano mojawapo ni ule wa kesi
ya Jamhuri dhidi
ya Iddi Mtegule
iliyotokea huko Dodoma. Katika
kesi hii vita ilikuwa kati ya Hakimu Mahakama ya Mwanzo na Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa
katika Mkoa wa Dodoma. Hakimu katika kutekeleza kazi yake alimwachia
huru mshtakiwa ambaye alikuwa ameshitakiwa
kwa kuuza maandazi.
Mkuu wa Wilaya alikasirika kwa mtu huyo kuachiwa huru
kwa kuwa alikuwa amepiga marufuku uuzaji wa vyakula ili kupunguza maambukizi ya
ugonjwa wa kipindupindu kilichokuwa kimejitokeza wakati huo, hivyo
aliamua kuandika
barua kali kwa
Hakimu akimuonya kwamba
ametoa maamuzi ya
upendeleo na majaribio ya makusudi kwa kuzuia juhudi
za mamlaka kuondokana na kipindupindu. Alikwenda mbali zaidi ya hapo kwa kumtaka hakimu kueleza
kwa nini alimwachia huru mshitakiwa na kutishia kuchukua
hatua kali dhidi yake. Hakimu huyu aliyekuwa anaielewa vizuri misingi
ya kazi yake alijibu
mara moja barua ya Mkuu wa wilaya na
kumueleza kwamba
alikuwa anaingilia huru wa mahakama. Alimweleza
zaidi kwamba si kila mshitakiwa anatakiwa
kuwa na hatia mpaka pale
itakapothibitika vinginevyo.
Pili,
mahakama inatakiwa iwe huru na wale wenye kesi mbele yake. Kila mwenye kesi
asimwingilie Jaji au Hakimu
anayesikiliza shauri lake.
Tatu, mahakama inapaswa iwe huru na
umma au sehemu ya umma. Hitaji hili nalo pia ni muhimu sana. Wananchi wanaweza wakaamini kuwa
mshitakiwa ni mhalifu kumbe mahakama ikamwona siyo. Sasa mahakama isishinikizwe
kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia. Uhuru huu ni muhimu sana
katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizo
kithiri za ufisadi ambapo baadhi ya wananchi tayari wamekwisha watia hatiani
baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya kufikishwa mahakamani.
Nne, Majaji na Mahakimu wanatakiwa
wawe na kinga katika kutekeleza majukumu yao.
Katiba ya sasa haiwapi maofisa hawa wa Mahakama kinga katika maamuzi
wanayofanya ya kusikiliza mashauri mbalimbali. Huu ni mwiba mkali sana katika tasnia nzima ya upatikanaji wa
haki nchini.
Tano, kuna uhuru binafsi wa kila Jaji
au Hakimu. Uhuru huu hupatikana kwa kumthibitishia kila jaji na kila hakimu
uhakika wa ajira yake. Jaji au hakimu ambaye ana wasiwasi na ajira yake na
anahofu kuwa ajira inaweza kukatishwa wakati wowote na kwa sababu yoyote,
hawezi kuwa thabiti katika kutekeleza majukumu yake ya utoaji haki chini ya
Katiba. Hii ni pamoja na uhakika wa kupata mshahara na maslahi yake kila mwezi
na kwa ukamilifu.
Pengine ni
wakati muafaka niseme kwamba dhana ya uhuru wa mahakama haimaanishi mahakama
kujitenga na taasisi nyingine za umma katika kulijenga taifa letu. Kumekuwepo
mtazamo na uelewa tofauti kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wananchi walio
wengi kwamba tunapozungumzia uhuru wa mahakama tunazungumzia utengano. Hii ni
uelewa potofu. Uhuru wa mahakama kimsingi ni uhuru anaopaswa kuwa nao Jaji au Hakimu
anapotekeleza majukumu yake ya utoaji haki na sii vinginevyo. Hivyo basi
inatosha kusema dhana ya uhuru wa mahakama ni ndugu pacha na jukumu la mahakama
la kikatiba la utoaji wa haki. Mahakama
huru ndio tegemeo kuu la Utawala wa Sheria.
Bila mahakama huru, Utawala wa Sheria utakuwa kama
ndoto za alinacha. Hata hivyo nitoe wito
kwa Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kwamba, uhuru wa
Mahakama unatudai tuwajibike kwa jamii, kwa kutoa haki sawa kwa wote na kwa
wakati. Tukifanya hivyo tutakuwa
kichocheo cha amani, udugu na uhuru.
Lakini pia heshima ya Mahakama itapanda na imani ya Umma kwa Mahakama
itaongezeka.
Wageni waalikwa mabibi na mabwana, msingi mwingine muhimu wa dhana ya utawala
wa sheria ni Mgawanyiko wa Mihimili ya Dola, yaani separation of powers.
Ibara ya 4 (1),(2),(3) na (4) ya Katiba yetu inaelezea mihimili mikuu mitatu ya
dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Ili kulinda na kuenzi dhana nzima ya
utawala wa sheria kama nilivyotangulia kusema, sharti mihimili hii isiingiliane
katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa taifa letu.
1.2 UMUHIMU WA
UTAWALA WA SHERIA NCHINI
Utawala wa sheria una umuhimu mkubwa sana nchini. Umuhimu wake kwa uchache ni kama ifuatavyo:-
1. Ukuzaji wa demokrasia:- Iwapo dhana ya
utawala wa sheria nchini utapewa umuhimu wake yamkini kutaimarisha demokrasia iliyopo nchini,
kutaimarisha na kudumisha amani na usalama kwa kila mwananchi. Kuheshimu
utawala wa sheria kutawawezesha wananchi kujikita kwenye shughuli za maendeleo
ya nchi.
Si vibaya nikasema wazi kuwa matukio mbalimbali
tunayoyaona na kusikia hivi sasa kama
migongano ya vyama vya siasa, migongano ya itikadi za kidini na maandamano
yasiyoisha yanatokana na kutokutii utawala wa sheria na kutoitumia demokrasia
tuliyonayo kwa ustaarabu.
2. Uimarishaji wa
Utawala bora:- Utawala wa
sheria ni muhimu kwa kuwa hupelekea utawala bora. Kwa kufuata misingi ya
utawala wa sheria Taasisi mbalimbali za kiserikali na idara zake zitachochea
misingi iliyotukuka ya utawala bora.
3. Upatikanaji wa
haki:- Iwapo misingi ya utawala wa
sheria itaheshimiwa na kuimarishwa ipasavyo jamii itapata haki
inayostahili. Watu wengi wamepoteza haki
zao na wengine kukumbwa na mauti kutokana na wanajamii kutokutii utawala wa
sheria.
4. Utawala wa
sheria kama kichocheo cha maendeleo:-
Maendeleo yoyote katika jamii yawe ya
kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni hayawezi kupatikana kama
utawala wa sheria utawekwa kapuni. Iwapo jamii itaheshimu dhana ya utawala wa
sheria maendeleo yatapatikana kwa kasi kubwa.
2.0 HALI HALISI YA
UTEKELEZAJI WA UTAWALA WA SHERIA NCHINI
Wageni
waalikwa, mabibi na mabwana,
utekelezaji wa dhana ya utawala wa sheria nchini unakabiliwa na matatizo lukuki
na changamoto mbalimbali. Baadhi ya matatizo na changamoto hizi ni kama zifuatavyo:-
1. Jamii
kujichukulia sheria Mikononi,yaani
“Mob Justice”, baadhi ya wananchi kwa kushindwa kuheshimu misingi ya utawala wa
sheria, wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi, pale wanapokamata mtuhumiwa wa
uhalifu. Hii kwa kiasi kikubwa hukinzana na misingi ya utawala wa sheria
iliyobainishwa katika Katiba yetu. Kwa mfano Ripoti ya Mwaka 2011 ya Kituo cha
Haki za binadamu, inaonesha ya kwamba mnamo mwaka 2011 idadi ya watu 673 waliuawa
nchini kote kwa aidha kuchomwa moto na au kupigwa kwa kutuhumiwa kutenda makosa
mbalimbali. Takwimu zinaonesha ya kwamba mikoa mitatu iliyoongoza kwa mauaji
hayo ni Dar- watu 157, Mbeya watu 89 na Mwanza watu 84 pia mikoa mitatu iliyokuwa
na mauaji kiasi ni mikoa ya Singida watu 5, Arusha watu 4 na Dodoma watu 3.
Ni wito wangu kwa wananchi na hasa vijana ambao
ndio taifa na viongozi wa kesho kuacha kabisa kujichukulia sheria mkononi.
Tudumishe amani, upendo na utulivu kwa kuheshimu utawala wa sheria.
2. Rushwa:- Rushwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa
utawala wa sheria nchini. Hayati baba wa Taifa wakati akilihutubia bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania tarehe 12 Oktoba, 1965
alisema “rushwa huzuia haki, na
kama ikiruhusiwa kuenea itaangamiza taifa letu. Haki inapouzwa na
kununuliwa, matumaini ya jamii yanapotea.
Nitoe wito na kuwakumbusha Majaji na Mahakimu kwamba huwezi ukapokea
rushwa ukabaki kuwa mwaminifu kwa kiapo cha Ujaji/Uhakimu. Yeyote anayepokea
rushwa hupoteza uhuru wake na anabakia kuwa mtumwa wa kudumu. Hata hivyo kuna wimbi la watumishi wa
Mahakama wengine kuacha Majaji na Mahakimu kudai rushwa tena kwa kutumia majina
ya Majaji na Mahakimu visivyo. Hili ni
baya zaidi na linahatarisha usalama wa Majaji na Mahakimu. Nichukue fursa hii kulikemea kwa nguvu na
niwatake wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
3. Kuingiliwa kwa uhuru wa Mahakama:- Kama nilivyoeleza hapo awali
serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikiingilia uhuru wa Mahakama. Vyombo vya
habari halikadhalika mara nyingi vimekuwa vikiingilia uhuru wa Mahakama kwa
kutoa taarifa za mashauri ambayo hayajamalizika mahakamani. Kumekuwepo uhaba wa
rasilimali watu na fedha. Vyote hivi vinapelekea kuingiliwa kwa uhuru wa
mahakama kwa njia moja au nyingine. Iwapo Mahakama haitakua huru haki haitaonekana
kutendeka. Katika shauri maarufu la Ally Juuyawatu dhidi ya Loserian Mollel & Mwenzake [1979] L.R.T. 6. Mhe. Jaji Edward Mwesiumo (kama alivyokuwa) alivamiwa ofisini kwake
kutokana na maelekezo ya “bwana mkubwa”,
na faili la kesi aliyokuwa akisikiliza kuchukuliwa kwa nguvu. Lakini
siku chache baadae faili hilo lilirudishwa na alipewa barua. Hata hivyo
kutokana na kuingiliwa na watendaji wa
serikali Mheshimiwa Jaji aliamua kujitoa kusikiliza shauri hilo.
Lakini pia wakati mwingine hata Katiba yetu
yenyewe, inazuia mahakama isifanye kazi yake kwa ufasaha, kwa mfano Ibara ya
7(2) inasema kwamba, nanukuhu “Masharti ya Sehemu hii ya Sura hii
hayatatiliwa nguvu ya kisheria na Mahakama yoyote. Mahakama yoyote nchini
haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya suala kama kutenda au kukosa kutenda jambo
kwa mtu au mahakama yoyote, au kama sheria, au hukumu yoyote, inaambatana na
masharti ya Sehemu hii ya Sura hii’’. Sehemu
hii inahusu “malengo muhimu na misingi
ya mwelekeo wa shughuli za serikali”. Hili ni hatari kubwa sana kwa dhana ya utawala
wa sheria nchini hususani katika msingi wa Uhuru wa Mahakama.
Wageni
waalikwa mabibi na mabwana, ili
kuondokana na changamoto hizi ni rai yangu kwamba yafuatayo yafanyike:-
a.
Elimu juu ya utawala wa sheria itolewe:- Napenda kutumia fursa hii kulipongeza jeshi la
polisi kwa kujitahidi kuelimisha umma juu ya utii wa utawala wa sheria katika
vipindi mbalimbali vya Radio na Televisheni chini ya kauli mbiu yao “ utii wa sheria bila shurti”. Hizi ni jitihada nzuri zinazotakiwa
kuungwa mkono na taasisi nyingine za serikali.
b.
Mabadiliko
ya Katiba:- Naelewa kwamba hivi sasa tuko kwenye mchakato kabambe
wa kuwa na Katiba mpya. Ni rai yangu kwa wananchi wote kuhakikisha wanachangia
maoni yao kwani mabadiliko haya yataleta mageuzi makubwa katika misingi
mbalimbali juu ya suala zima la utawala wa sheria nchini.
c.
Uboreshwaji
wa Mhimili wa Mahakama, kimiundombinu na stahili za wafanyakazi:- Miundo
mbinu ya Mahakama zetu sio rafiki na wahitaji wote wa haki na hata kwa watoaji
haki wenyewe. Maslahi duni pia hufifisha
hamu ya kufanya kazi kwa bidii.
d.
Kurekebishwa kwa sheria kandamizi:- Sheria kandamizi zinaondoa dhana ya kuleta haki
kwa watanzania wote mbele ya sheria. Sambamba na uwepo wa Katiba mpya ni
dhahiri kwamba sheria kandamizi zinapaswa kufanyiwa marekebisho, kama siyo
kufutwa kabisa.
e.
Uzingatiaji wa dhana ya mgawanyo wa madaraka katika utekelezaji wa shughuli za
serikali nchini, nk.
f.
Kutoa kipaumbele kwa makundi yaliyo pembezoni, ili makundi hayo nayo yaweze kufaidi keki ya taifa”
national cake” kama yalivyo makundi mengine.
3.0 MWISHO
Wageni
waalikwa mabibi na mabwana napenda
kuhitimisha kwa kusema kwamba hakikisho la kuwepo haki sawa kwa wote katika nchi yetu ni uwepo wa Utawala wa
Sheria. Kama
nilivyojitahidi kuonyesha hapo juu, msingi mkuu wa Utawala wa Sheria ni uwepo
wa Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wake bila woga, chuki wala
upendeleo. Kwa hiyo basi sote tudumishe
Utawala wa Sheria. Aidha nichukue fursa
hii kuwaasa watanzania wenzangu kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba,
ili tupate Katiba nzuri tuitakayo kwa maendeleo ya nchi yetu nzuri na vizazi
vijavyo.
Asanteni kwa kunisikiliza!!
Mungu ibariki Mahakama, Mungu ibariki
Tanzania.